Hafla ya makabidhiano ya vitabu vilivyotolewa na mradi wa ‘Soma Japani’ (READ JAPAN PROJECT)

2025/4/9
hotuba ya balozi
cheti
vitabu

Tarehe 8 Aprili, 2025, hafla ya makabidhiano kwa ajili ya "READ JAPAN PROJECT", mradi wa kuchangia vitabu ili kukuza uelewa kuhusu Japani, ilifanyika katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Prof. Nelson M. Boniface, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utafiti), Prof. Kelefa Mwantimwa, Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba, na Mheshimiwa Yoichi Mikami, Balozi wa Japani, pamoja na wafanyakazi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

"READ JAPAN PROJECT", inayoungwa mkono na Wakfu wa Nippon (The Nippon Foundation), na kutekelezwa na Wakfu wa Tokyo (The Tokyo Foundation), inalenga kukuza hamu na uelewa kuhusu Japani kwa kutoa vitabu vinavyohusiana na Japani kwa maktaba na taasisi za utafiti kote ulimwenguni. Hadi sasa, takriban vitabu 98,000 vimetolewa kwa taasisi zaidi ya 1,400 katika nchi zaidi ya 150, na huu ni mchango wa pili kwa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (ya tatu ikiwa ni pamoja na Chuo cha Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).

Balozi Mikami alitoa pongezi kwa hafla hiyo na kutaja kuwa uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu kati ya Japani na Tanzania umefanikisha mchango huo na kusoma ujumbe wa Mwenyekiti wa Wakfu Nippon Dk. Yohei Sasakawa. Katika ujumbe wake, Mwenyekiti Sasakawa aliangazia uhusiano wake wa muda mrefu na Tanzania na juhudi zake za kutokomeza ugonjwa wa ukoma na kueleza matumaini yake ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili kupitia mabadilishano ya kielimu na kitamaduni.

Inatarajiwa kuwa vijana wa Tanzania wataongeza uelewa wao kuhusu Japan kupitia vitabu vilivyotolewa na kuwa daraja kati ya nchi hizo mbili.