Mkutano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Japani na Tanzania

2025/8/22
mkutano1
mkutano2
1. Mwanzoni mwa mazungumzo, Waziri Iwaya alieleza kuwa angetamani kuimarisha zaidi uhusiano katika nyanja mbalimbali na Tanzania, ambayo ina uwezo wa kuwa na uchumi mkubwa, na inatumika kama lango kwa kampuni za kijapani zinazoingia Afrika Mashariki. Kwa upande wake, Waziri Kombo alitaja umuhimu wa TICAD kwa Tanzania na kwamba anathamini sana msaada wa Japani, na akaonesha dhamira yake ya kuendeleza zaidi uhusiano wa pande mbili na ushirikiano katika masuala ya kimataifa.

2. Baada ya hapo, Waziri Iwaya alionyesha kufurahishwa na kutiwa saini kwa Hati ya Ushirikiano kuhusu uendelezaji wa rasilimali watu katika sekta ya ujenzi na kueleza dhamira yake ya kuchangia katika vipaumbele vya Tanzania kuhusu maendeleo ya rasilimali watu na uendelezaji wa kilimo. Waziri Iwaya pia aliomba ushirikiano katika kuhakikisha mazingira ya uchumi yenye haki na uwazi, akirejelea changamoto zinazozikabili kampuni za kijapani zinazoingia Tanzania. Waziri Kombo alijibu kwa kueleza juhudi za Tanzania katika kuboresha mazingira ya kiuchumi na akaeleza matumaini yake kuwa kampuni za kijapani zitaongeza uwekezaji wao nchini Tanzania, katika sekta kama vile teknolojia mpya, madini na kilimo.

3. Mawaziri hao wawili walibadilishana maoni na walikubaliana kushirikiana kwa karibu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na sera zao kuhusu Korea Kaskazini, masuala ya nyuklia na makombora, na suala la utekaji nyara, pamoja na mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.